Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia, ambapo sambamba na kuishukuru Russia kwa ubunifu wake wa kuanzisha mchakato wa Iran kupatiwa uanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, amesema, hatua hiyo inaimarisha uhusiano wa karibu mno uliopo kati ya Tehran na Moscow.
Seyyid Ebrahim Raisi amegusia pia mashirikiano iliyotoa Russia kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya corona na juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kutengeneza na kuzalisha chanjo ya pamoja ya corona baina yake na Iran na akabainisha kwamba, kutokana na mazingira maalum yaliyopo hivi sasa, Iran inahitaji kupatiwa shehena zaidi za chanjo ya corona.
Rais Ebrahim Raisi aidha amesema, kama ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaheshimu na kutekeleza mikataba ya kimataifa ukiwemo unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT, imeazimia pia kwa dhati kuhakikisha inadhamini haki ya wananchi wake ya kunufaika na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na kufaidika na matunda ya teknolojia hiyo katika nyuga zote.
Halikadhalika ameashiria matukio ya Afghanistan na akasema, kurejesha amani, usalama na utulivu nchini Afghanistan ni jambo linalotiliwa mkazo kila mara na Iran; hivyo makundi ya Kiafghani inapasa yashrikiane kwa ajili ya kurejesha uthabiti nchini humo haraka iwezekanavyo na kukutumia kuondoka Marekani kama fursa ya kipekee ya kurejesha amani na uthabiti wa kudumu nchini humo.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, kustawisha uhusiano na Iran kuna umuhimu mkubwa kwa Russia na akaeleza kuwa, anakaribisha pendekezo la kufunga mkataba kamili wa mashirikiano ya pande mbili.
Kuhusu mchakato wa kukabidhi chanjo ya corona kwa Iran, Putin amesema mchakato huo utaendelea kwa kasi kubwa zaidi kuanzia mwezi ujao wa Septemba.
Kwa upande wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran, Rais wa Russia ameeleza bayana kwamba, JCPOA hayawezi kufanywa mateka wa matatizo ambayo hayana uhusiano na makubaliano hayo ya nyuklia.../
342/